Thamini Thawabu Zako | ThawabCurrency Pt. 2
Muendelezo wa Namna ya kuthamini na kuzilinda Thawabu zako na kujiepusha Na vitendo vyenye kupoteza Thawabu zako..
Bismillah..
Assalam alaykum warahmatullah..
Karibu ndugu yangu katika makala hii. Tulieleza katika makala iliopita namna ya kuzithamini Thawabu zetu kama tuvozithamini pesa au Mali zetu.
Na huu ni muendelezo wa makala hio Kwan vitu vinavofanya tupoteze thawabu zetu ni nyingi.. Na Allah atuepushe navo..
Ikiwa hukuisoma makala iliopita basi usijali, nitakuekea link mwisho. Hivo soma hii mpaka mwisho, na Allah akupe ufahamu na atupe utekelezaji. Amiin!
Kutokumtii Allah na Mtume Salallahu alayh wa salam..
Miongon mwa sababu zinazopelekea tupoteze thawabu zetu baada ya kuzihangaikia katika Ibada ni kutomtii Allah katika yale aliotuamrisha na kutoacha yale aliotukataza..
Na kutokumtii Rasulullah Salallahu alayh wa salam katika yale aliotuelekeza..
Anasema Allah katika Qur’an..
{ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَلَا تُبْطِلُوا أَعْمَالَكُمْ }
[Surah Muhammad: 33]
Enyi mlio amini! Mt'iini Allah, na mt'iini Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu.
Kwahivo tunaona katika Aya hio, Allah anatuamrisha tumtii yeye na Mtume wake na wala tusiviharibu vitendo vyetu kwa kupotea kwa Thawabu zake kwa uasi..
Maneno machafu na kauli mbaya..
Maneno machafu na kauli mbaya kwa majirani na jamaa kama vile kusengenya, kuteta, matusi na kadhalika katika maneno mabaya humfanya mtu apoteze Thawabu zake hata kama atajikita kiasi gani katika Ibada..
Anaeleza Rasulullah Salallahu alayh wa salam katika hadith
Imepokelewa katika riwaya ya kwamba mwanamke mmoja katika zama za Mtume (s.a.w.w) tangu asubuhi hadi jioni alikuwa akijishughulisha na ibada bila kupumzika, na katika masiku mengi ya mwaka alikuwa akifunga..
lakini mwanamke huyo alikuwa na kasoro moja, nayo ni kuwa tabia yake ilikuwa ni mbaya na alikuwa akimuudhi jirani yake kwa ulimi wake mbaya,
Mtume (s.a.w.w) akasema kuhusina na mwanamke huyo: Hakuna kheri yoyote kwa mwanamke huyo..
Kwa hivo ni vyema kulinda ulimi wako ili kulinda Mali yako, Thawabu, Mali yako ya thamani..
Waliojiwekea Juhudi zao zote katika kutafuta Dunia..
Unaweza baada ya kuona kichwa hicho ukashtuka, kutafuta Dunia tena!?, kivipi?
Relax, nikuelezee ndugu..😄
Kipengele hichi kinawahusu wale ambao nguvu zao, Juhudi zao na harakat zao ni hufanya kwa ajili ya Dunia na si vinginevo..
Hufanya na hujitaahidi ili Dunia yao ipendeze na hawajali kuhusu Akhera wakiwa katika shughuli zao..
Mfano, mtu anaweza akawa na Biashara yake, kuhusu biashara hio, Allah amempa muongozo namna gani aifanye biashara yake kuepusha kula haram na pia imemuonesha Uislam kuhusu atakachokipata katika biashara ile vipi akitumie..
Lakini yeye kwakuwa malengo yake ni Dunia hatojali anapataje chumo lake na wala hajali vipi atalitumia..
{ الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا }
[Surah Al-Kahf: 104]
Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri.
{ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا }
[Surah Al-Kahf: 105]
Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu.
Kwa hivo ni vema mambo yako hata yale unayoyaona si katika Mambo ya Ibada ila yaendee kistaarabu na iwe Lengo ni kwa ajili ya Akhera..
Sijui umenielewa Akhy?, Ikiwa bado hujanielewa nitaweka namba zangu mwishon. Nitafute WhatsApp niambie ambapo hujaelewa..
Husda..
Naam, jambo la mwisho katika makala hii ambalo linaweza kukupotezea Thawabu zako za thamani ni Husda, nayo ni kuchukia Neema alizopewa ndugu yako na Allah subhana. Au pia kutaka Neema ya fulan alionayo ndugu yako imuondokee..
Na Hali hii tunayo mno Allah atuepushie..
Anasema Rasulillah Salallahu alayh wa salam..
Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Allaahu 'anhu):
Amesema Mtume Rehma na amani ziwe juu yake:
Jihadharini na husuda, kwani huteketeza matendo mema kama vile moto unavyoteketeza kuni au nyasi.
[Chanzo: Sunan Abi Dawud 4903, Daraja: Hasan (haki) kwa mujibu wa Ibn Hajar (Rahimahullah)]
Kabla sijamaliza..
Kabla sijamaliza, nikuongezee maneno haya Akhy/ukhty yangu..
Kuwa jambo hili la kuzipa Thamani Thawabu zako na kuzihifadhi, kuzizalisha na kuzikuza, linaweza liwe gumu kwako..
Kwakuwa Pesa ikipotea unaona umepoteza kaisi gani, umeingiza kiasi gani.. Ila kwa Thawabu huwezi kuona kwa dhaahir.
Ila ni muhimu kwako kuwa na Yaqini isiyo na shaka kuwa unalipwa ukifanya tendo jema..
Na hivo jitaahid unapofanya tendo jema, linda Thawabu zilizopatikana kwa tendo hilo kwa kujiepusha na riyaa, na ufanye kwa ikhlaas lillah..
Pia zikuze Thawabu kwa kufanya matendo mema zaidi. Na hakika, unapojiona unazidi kupata hamu ya kufanya mema, basi ujue hio ni dalili ya kukubaliwa matendo..
Ibn Rajab akasema: "Ishara ya kwamba matendo mema yako yamekubaliwa ni kwamba unafanya mema zaidi baada yake."
[لطائف المعارف صحفة ٩٣]
Mwisho jiepushe na kutokufanya matendo ambayo huenda ukapoteza amali zako na Thawabu zako, na Allah atuongoze sote, Amiin..
Ni Mimi Al Akh, Mubaarak
Assalam alaykum..
Ikiwa hukuisoma Thawabu Currency Part 1. Basi bofya hapo chini..
Ikiwa una swali, maoni, ushauri au kuna kheri unahitaji kunifikishia, basi nitafute WhatsApp.