Tiba Ya Uhakika Ya Kuuchunga Ulimi Ni Hii..
Bismillah Ar Rahman Ar Raheem..
Assalam alaykum ndugu na karibu katika makala hii inayoletwa kwako na Ahadun Ahad studio.
Ni Mimi Al Akh. Mubaarak.. Na Leo Biidhnillah, Tunaongelea Tiba Halisi ya kuweza Kuchunga ndimi zetu katika kutamka maneno maovu na machafu..
Ikiwa ni mara yako ya kwanza katika makala zetu hizi basi usiache kusubscribe ili usikose Faida kama hizi hapo baadae In Shaa Allah..
Utangulizi..
Naam..
Miongoni mwa vitu ambavo Rasulullah Salallahu alayh wa salam ametuusia mno ni kuchunga ulimi..
Kuuchunga kutokana na maneno machafu, husda, hasira na maneno ya karaha..
Ila ukweli ni kwamba Tiba halisi ya kuuchunga ulimi, si kuuchunga ulimi..
Labda nikupe mfano rahisi..
mfano ikitokea umevunjika mguu, ukipewa dawa za maumivu pekee bila kuungwa mguu unaweza ukapona maumivu lakin hio si Tiba halisi..
Ila Tiba halisi ni kuungwa mguu hata bila kupewa dawa za maumivu utapona..
Hivyo, hatutaweza kuchunga ndimi zetu hivi hivi tu kwa kuamua kunyamaza pekee, Ila kuna kitu inabidi ukitibu kwanza ndo utaweza kuuchunga ulimi wako..
Ulimi ni kama muwakilishi wa hicho kitu, ikiwa hicho kitu kimechafuka, basi ulimi hautaweza kuwa msafi, na kama hicho kitu kimesafika, basi ulimi nao utakuwa msafi..
We unadhani ni kitu gani hicho?😃
Hakika kitu hicho ni Moyo..
Uhusiano Wa Moyo Na Ulimi, Maradhi Ya Moyo..
Kama nilivosema mwanzo kuwa ulimi unao uhusiano na moyo.. Kile ambacho kipo moyoni ikiwa ni unafiki, chuki au Husda, itatoka Tu na kujidhihirisha kupitia ulimi..
Na kama mtu ana moyo Safi hata kauli zake zitakuwa Safi..
Na haya ya ndimi kudhihirisha Kilichopo moyoni ni miongoni mwa kazi zake Allah Subhanahu wa taala..
Kama Allah anavoeleza katika Qur’an..
{ أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ أَنْ لَنْ يُخْرِجَ اللَّهُ أَضْغَانَهُمْ }
[Surah Muhammad: 29]
Je! Wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Allah hatazidhihirisha chuki zao za ndani(na yale yalioficha nyoyo zao)?
Naam, Aya hii inaanza kutueleza kuwa moyo ndo kitu ambacho huugua, na kupelekea ulimi nao kuchafuka na kuugua..
Na maradhi ya moyo hapa si Pressure, wala heart failure, wala sio Mycardio infarction..😁
Maradhi ya moyo hapa, ni matamanio, wasiwasi na Mashaka juu Haki(Qur'an na Uislam), chuki, unafiki, na Husda n.k..
Yani ikiwa mtu ana chuki na Uislam na Sheria zake au Qur’an, au ana Husda na wewe, utajua Tu.
Kama ana chuki, unafiki, upendo au matamanio, au hasira, yani chochote tu katika maradhi ya moyo hatoweza kuyaficha, Ila Allah atayadhihirisha..
Atayadhihirisha vipi?, Ndo anaendelea kutueleza Allah..
{ وَلَوْ نَشَاءُ لَأَرَيْنَاكَهُمْ فَلَعَرَفْتَهُمْ بِسِيمَاهُمْ ۚ وَلَتَعْرِفَنَّهُمْ فِي لَحْنِ الْقَوْلِ ۚ وَاللَّهُ يَعْلَمُ أَعْمَالَكُمْ }
[Surah Muhammad: 30]
Na tungeli penda tungeli kuonyesha hayo na ungeli watambua kwa alama zao; lakini bila ya shaka utawajua kwa namna ya kauli zao. Na Allah anavijua vitendo vyenu..
Naam, katika Aya hio Allah anatuambia, utawajua kwa namna ya kauli zao. Yaani namna anaongea na wewe, reactions zake kwako, anavokutreat katika miamala yenu n.k..
Na hii ni kuwa hata kama atajitaahid kutodhihirisha hisia zake kwako, Ila Allah atayadhihirishia yote kwako siku moja..
Hivo, Ikiwa unahitaji uweze kuchunga ulimi wako, na ikiwa unahitaji kutibu ulimi wako.
kwanza ni uutibu moyo wako juu ya maradhi yake..
Ukifanya hivo basi kuchunga kwako ulimi itakuwa ni rahisi sana, na Allah atakuongoza zaidi..
Sasa je, ni ipi tiba ya Maradhi ya Moyo?
Jibu hili hapa..
Tiba Ya Uhakika Ni Hii..
Anaeleza Sheikhul Islaam Ibn Taymiyyah katika kitabu chake Amraadhul Quluub wa Shifaauhaa (Maradhi Ya Moyo na Tiba zake).
Sheikh anasema tiba za moyo kama ifuatavyo..
Tiba ya kwanza, Qur’an..
Qur’an ni tiba ya yale yaliyomo ndani ya moyo, na kwa yule ambaye ana maradhi ya shaka na matamanio moyoni mwake, kwani ina dalili zilizo wazi zinazotofautisha haki na batili, na huondoa maradhi ya mashaka na uwongo kwa kuacha elimu na utambuzi sahihi na ufahamu kiasi ambayo moyo huona mambo kwa mujibu wa uhalisia wake..
Na hivo mtu ambae anajitaahidi katika kumtaja Allah na kumkumbuka, anakuwa yupo katika tiba za kuufanya moyo uwe safi na utulie..
Na moyo ukitulia automatically ulimi utatulia..
Na hakuna Dhikr inayotuliza moyo vizuri kama Qur’an..
Kama Allah anavotueleza..
الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُمْ بِذِكْرِ اللَّهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ }
[Surah Ar-Ra`d: 28]
Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Allah. Hakika kwa kumkumbuka Allah ndio nyoyo hutua!
Tiba ya pili, Kufanya matendo mema zaidi kama Zakah na Sadaka..
Zakah maana yake ni utakaso katika lugha, tafsiri yake ni: kukua na kuongezeka kwa usahihi wake kama inavohitajika, kwa mfano utasema, 'kitu kina zaka', wakati kimekua katika usahihi wake..
Moyo unahitaji kulelewa ili upate kukomaa na kuongezeka mpaka ukamilike na kusahihishwa sawa kama vile mwili unavyohitaji chakula chenye manufaa kwake..
Lakini pamoja na hayo ipo haja ya kuzuia jambo lolote lisiudhuru..
Hivo Zakah yako utakayoitoa itakuwa ni miongoni mwa vitu vinavousafisha moyo wako na kuustawisha..
Na kuuepusha na madhara, maradhi yenye kuuharibu..
Pia katika maana zingine za Zakah ni hii..
Maana yake Zakaa, ni Tawhid na Imaan ambayo kwayo moyo hutakasika, kwani tawhid ni pamoja na kukataa Uungu wowote badala ya Allah na kuthibitisha ubwana wa Allah pekee moyoni..
hii ikiwa ni hakika ya 'La Ilaha Illa Allah' (hakuna apasae wa ibada isipokuwa Allah) na huu ndio msingi wa kuzitakasa nyoyo.
Na sadaqah, kutokana na kuzima kwake madhambi kama vile maji yanavyozima moto, husababisha moyo kutakasika..
Tiba ya tatu, Kuacha matendo mabaya na maovu kwa kutubia kwa Allah..
Vile vile kujiepusha na matendo machafu na dhambi hupelekea utakaso wa moyo, kwa kuwa haya ni ya kiwango sawa na ukoma wa mwilini au miiba kwenye ua..
mtu anapotaka kutubia dhambi, moyo huachiliwa kutokana na uchafu - ambapo ulichanganya vitendo vyema na vitendo viovu..
Basi mtu anapotubu kutokana na dhambi, nguvu ya moyo hujitokeza kwa kutamani kwake kufanya vitendo vyema na hupata nafuu kutokana na mambo ya uwongo na ya kifisadi ambayo yalizama ndani ya moyo..
Naam, hizo ndo Tiba za kuutakasa moyo kutokana na maradhi yake, utazipata kuanzia ukurasa 54 - 58 wa kitabu..
Ikiwa utahitaji kitabu hicho, ninayo softcopy yake kwa Lugha ya Kiingereza, hivo usisite kunitafuta kwa WhatsApp nikutumie..
Namba nitaweka mwishoni..
Nimalizie..
Sina mengi wallah, Allah azitakase nyoyo zetu ili tuweze kuepusha ndimi zetu na kusema yasiyofaa..
Allahumma amiin..
Ni Mimi Al Akh Mubaarak..
Kutoka Ahadun Ahad Studios..
Assalam alaykum..
Usiache kusubscribe kama hujasubscribe, ili usikose Faida Tele..🙂
Pia ikiwa una maoni, ushauri, nasaha, au hata salamu. Zifikishe kupitia namba yangu ya WhatsApps. Hakika nafurahi kuona ukinitafuta..
Nijulie hata hali Muislam mwenzio..😄