Kitu Kimoja Cha Kukithamini Kama Pesa, au Zaidi.. | ThawabCurrency Pt.1
Katika Ulimwengu Wetu Huu, Pesa ni yenye kupewa thamani zaidi. Lakini kipo kitu kimoja (1) kinachotakiwa kupewa thamani kama tunavoithamini pesa. Ni kitu gani?, Shuka nami..👇🏼
Bismillah Ar Rahman Ar Raheem
Assalam alaykum warahmatullah wabarakatuh..
Naam, karibu tena katika makala hii kutoka Ahadun Ahad Studio, ikiandikwa na Mimi Akhy yako Mubaarak.
Ikiwa ndo mara yako ya kwanza kusoma makala hii kutoka kwangu, basi nikunasihi usubscribe hapo chini ili usiweze kukosa Faida kama hizi siku za usoni kutoka kwetu. Na Allah atupe hidaya, Amiin!
Naamin umefika hapa ukihitaji kujua kitu gani hicho chenye thamani zaidi ya pesa?, Ama sivo ndugu?😃
Maana katika ulimwengu wetu huu wa sasa Pesa ndo kila kitu, tunaweza kusema hivo..
Ukiwa nazo, utapata nyingi heshima, thamani, na utakuwa mbora wa watu..
Na kwasababu hio, tunajitaahid kuichuma Mali kwa Jasho, kuitunza, kuithamini, kuthamini kile kitachotupa mali, ikiwa ni kazi au biashara, tunajitaahid kuiwekeza, kuizalisha na kadhalika..
Na ndo ikaja misemo kama “Tafuta hela”😄
Hakika Pesa ni ya muhimu mno katika maisha yetu..
Sasa, siku moja niliwaza jambo, kuwa
Hivi Kwanini nisizithamini Thawabu zangu kama vile ninavozithamini pesa zangu..?
Yani iwe, kama unavothamini pesa na kuitafuta basi, uithamini Thawabu na kuitafuta..
Uwe na sarafu mbili za kuzithamini katika maisha yako, sarafu ya pesa na sarafu ya Thawabu..
Unaweza jiuliza, sasa Al Akh Mubaarak, kwanini niilinganishe Thawabu iwe sawa na pesa?🤔
Basi jibu ni hili ndugu..
Kama ambavo pesa hupanda thamani na kushuka, pia Thawabu hupanda thamani na kushuka.
Kama ambavo Pesa hutafutwa, na Thawabu pia hutafutwa..
Kama ambavo pesa hutunzwa, na Thawabu pia hutunzwa..
Kama ambavo pesa hupotea, na Thawabu pia zinaweza zikapotea baada ya kuvunwa..
Kama ambavo pesa huzalishwa kupitia mtaji mdogo na ikakuzwa, na Thawabu pia ni hivo hivo.. Kama ambavo pesa huwekezwa, na Thawabu pia huwekezwa..
Umeanza kunielewa ndugu..🙂
Hicho ndo nilichokuwa namaanisha katika kuthamini Thawabu zako kama unavothamini Pesa zako, kwasababu Thawabu ina sifa sawa na pesa..
Kupanda thamani kwa Thawabu na kushuka kwake..
Kufuata Sunnah
Thawabu hupanda thamani ikiwa utafanya matendo kwa kufuata Sunnah ya Mtume salallahu alayh wa salam kama ambavyo ameelekeza..
Yani katika kila Ibada, kuna nguzo za muhimu za kufanya na kuna sunnah za kufanya..
Ukifanya nguzo peke ake utalipwa lakini ukifanya nguzo na Sunnah zote utalipwa zaidi. Hivo utakuwa umezipa thamani ujira wako..
Na ukiacha kufanya matendo kwa kufuata Sunnah utapunguza thamani ya Thawabu. Hivo zitashuka..
Kwahivo tujiepushe na zile kauli za "Ukifuata sunnah unapata Thawabuu, usipofuata hupati dhambiii.."🗣️👌🏼
Ni kweli, Lakin we hutaki matendo yako yawe na thamani zaidi?
Kukosa Khushuu’ (Utulivu katika Ibada)
Jambo lingine linaloshusha thamani ya Thawabu katika matendo, ni ikiwa tutazifanya amali zetu bila خشوع,Khushuu'
Yani kutulizana kwa akili na moyo katika Ibada, au swaumu ukaifunga na huku wafanya matendo kama kusengenya, na vitendo vingine vilivokatazwa..
Kuzipoteza au kuharibika kwa Thawabu baada ya kuzivuna..
Kama vile ambavo watu hupoteza pesa zao kwenye kamari huko, na kwingine..
Basi hata Thawabu, mtu anaweza zipoteza hivi hivi baada ya kuzihangaikia katika Ibada..
Na miongoni mwa mambo mtu akifanya atapoteza Thawabu zake ni haya..
Riyaa..
Riyaa ni kufanya Ibada au kuitengaza ili watu wakuone, wakusifie n.k.. Hivo inakuwa hujaifanya kwa ajili ya Allah, na ukifanya hivo, basi Thawabu zako utakuwa umezipoteza na utakuwa hukulipwa chochote..
Kama anavotueleza katika Aya hii..
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُمْ بِالْمَنِّ وَالْأَذَىٰ كَالَّذِي يُنْفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ…
Enyi mlio amini! Msiharibu (Thawabu za) sadaka zenu kwa masimulizi na maudhi (ya kutangaza), kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu..
[Baqara 2:264]
Hivo chunga Nia na ikhlaas yako katika Ibada, au kitendo chochote usikifanye isipokuwa utaraji malipo kwa Allah pekee na si kwa watu au vinginevo..
Dhulma..
Kiukweli Dhulma zipo za aina nyingi mno, lakini Dhulma kuu zaidi ni..
1. Kumshirikisha Allah..
Katika vitendo ambavo ukivifanya unaweza ukapoteza sarafu zako za Thawabu ulizozichuma kwa muda mrefu katika Ibada ni shirk..
Na shirk, ni kumuabudu asie kuwa Allah, au kumfanya Allah kuwa na mshirika katika uzungu wake..
Kama Allah anavotueleza kuhusu kupotezea kwa Thawabu endapo utamshirikisha..
لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ
ukimshirikisha Allah a'mali zako zitaanguka (zitapotea) na utakuwa miongoni mwa waliokhasirika..
[Az Zumar : 65]
2. Kumdhulumu mtu kwa kumsengenya, kumvunjia heshima yake na utu wake..
Kama anavoeleza Rasulullah kuwa siku ya Qiyama Thawabu za mtu huyo mwenye kudhulumu atapewa yule aliemdhulumu kama fidia(faini)..
Rejea : Ṣaḥīḥ al-Bukhārī 2449
Unafiki
Miongoni mwa sifa cha mtu mwenye unafik katika moyo wake huchukia baadhi ya maamrisho ya Allah na kuacha kuyatekeleza, na kupenda kufanya yale yanayomchukiza Allah..
Hivo ukiwa na sifa, chunga. Huenda ukabatilisha matendo yake uliojitahid kuyafanya na ukapoteza Thawabu zako nyingi..
Kama anavotuelezea Allah..
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ }
Hayo ni kwa sababu walifuata yaliyo mchukiza Allah na wakachukia radhi yake, basi akabatilisha vitendo vyao.(kwa kupoteza Thawabu zao)
[Muhammad 47:28]
Hayo ni baadhi ya matendo ambayo mtu akiyafanya anaweza zipoteza Thawabu zake na akawa katika hasara..
Hivo jichunge na jiepushe nayo, nitaelezea matendo mengine yanayopoteza Thawabu zetu katika makala ijayo In Shaa Allah..
Kuzizalisha Thawabu, na kuziwekeza..
Kuzizalisha Thawabu
Thawabu huweza kuzalishwa kwa kufanya tendo dogo na kupata ujira mkubwa kama vile kutoa Sadaka ima ya mali, au nguvu zako katika kufanya dini ya Allah isonge
Kama anavosema Allah..
{ مَثَلُ الَّذِينَ يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنْبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنْبُلَةٍ مِائَةُ حَبَّةٍ ۗ وَاللَّهُ يُضَاعِفُ لِمَنْ يَشَاءُ ۗ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ }
[Surah Al-Baqarah: 261]
Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Allah ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Allah humzidishia amtakaye, na Allah ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.
Kuwekeza Thawabu
Na ukawekeza Thawabu zako kwa kufanya kitendo na ukaendelea kulipwa hata baada ya kufa.
Kama vile kujenga kisima, Msikitin au kupanda mti ili kutarajia malipo kwa Allah na kutaraji watu wapate Faida kwa kheri Ile endelevu..
Pia kufundisha elimu ambayo itamfanya mtu awe karibu na Allah, au kumkuza mtoto mwema atakaekuombea dua na msamaha baada ya kufa..
Kama anavoeleza Rasulullah Salallahu alayh wa salam katika hadith iliopo katika Riyad as-Salihin 1383.
Kuzitunza Thawabu..
Utaweza kuzitunza Thawabu zako za thamani kwa kujitaahidi kujiepusha na vyenye kubatilisha na kuharibu Thawabu kama nilivozieleza hapo juu na pia kuendelea kufanya matendo mema yenye ujira mkubwa..
Pia ni vema sana ujihesabu matendo yako, ukae na upige mahesabu juu ya matendo yako na Thawabu zako, umeingiza Thawabu kwa matendo yapi, umepoteza Thawabu zako kwa yapi na kwanini?
Kwakuwa Thawabu zako ndo mchongo wako huo wa kupata Akhera..😄
Yani kama vile unavopiga mahesabu ya Mali yako na Biashara yako..
Kama vile Umar Ibn Khatab ( Radhiyallahu anhu) alivosema : “Jihesabu (mwenyewe matendo yako) kabla haujahesabiwa ( siku ya Qiyama)..”
[Tirmidhi]
Nikimalizia..
Kama ambavo unathamini Kazi, biashara zako..
Thamini pia kile kinachokupa thawabu, ikiwa ni Salaa, swaumu, Dhikr, kutafuta elimu n.k
Hio ndo biashara yako, mchongo wako na Allah, ili akupe thawabu..🙂
Na hakuna biashara ambayo utafanya na Boss, Allah kwa ikhlaas lillah, na ukataraji malipo na asikulipe vizuri.
Kama anavowapa bishara njema wale ambao wamefanya biashara nae..
وَمَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّهِ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُمْ بِهِ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيم
Na nani atimizae ahadi (ya kulipa vizuri) kuliko Allah? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
[At Tawbah : 111]
Naam, sijamaliza bado. Ila nahofia kukuchosha. Nadhani ujiandae na makala ijayo nitaendelea kuelezea yanayofilisi sarafu zetu za Thawabu, Thawabu Currency yetu..
Muendelezo wake upo hapa..
Na unaweza ukawasiliana nami Kwa WhatsApp, bonyeza hapo chini..
Sina la zaidi, Ni Mimi Mubaarak, kutoka Ahadun Ahad Studio..
Assalam alaykum..
Jazakallahu khayr..